Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Othman Chande akikagua gwaride wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika Dar es Salaam, mwaka huu. Picha ya Mtandao
Dar es Salaam. Mahakama ni chombo kilichoanzishwa, kwa mujibu wa Katiba na chenye mamlaka kisheria ya kutoa haki katika jamii kuhusu mashauri mbalimbali ya kijinai, mauaji au madai ili mkosaji aadhibiwe na asiye na hatia aachiwe.
Katiba imeruhusu kuanzishwa kwa mahakama katika ngazi mbalimbali kuanzia mwanzo, wilaya, mkoa, mahakama kuu na rufani. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kwamba katika baadhi ya mahakama za mwanzo za jijini Dar es Salaam kuna mitandao ya rushwa inayoshirikisha wanasheria feki, polisi na mahakimu kukosesha haki.
Mitandao hiyo inaathiri utoaji hukumu, inachangia kuchelewesha kesi kwa makusudi, ulaghai katika kuwatoa watuhumiwa waliopo mahabusu, rushwa ili dhamana itolewe na kulazimishwa kumaliza kesi kabla ya hukumu. Baadhi ya watu wanaoonekana kuwa wagumu kutoa fedha za kinachoitwa “kusukuma mwenendo wa kesi” hupewa usumbufu kama vile kulazimishwa kufika asubuhi mahakamani wakati kesi zao zinasomwa au kusikilizwa jioni au kuahirishwa.
Mtandao wa dhuluma
Muhidini Ngulumwa aliyeshitakiwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Magomeni, alisema kuwa ni mwaka wa tatu tangu aliposhitakiwa, lakini kesi yake inatajwa na hajawahi kupanda kizimbani. Japokuwa kuna wakati huwa anamwona kortini mlalamikaji wakati wa kusikilizwa kesi huambiwa mlalamikaji huyo ana udhuru hivyo kesi huarishwa kwa mtindo huo.
Ngulumwa alisema anashangaa kwa nini mshtaki anakosekana mahakamani zaidi ya mara tano lakini kesi hiyo haifutwi huku akiendelea kutumia fedha kwa nauli.
“Kuna Mzee wa Baraza aliwahi kuniambia nikitoa fedha hiyo kesi itamalizika mapema na hukumu itakuwa upande wangu. Nilipomuuliza kiasi gani aliniambia Sh500,000, ili agawane na wenzake na Sh200,000 apewe hakimu. Nilipomjibu sina sijamuona hadi leo na bado napoteza muda huku hatima yangu nikiwa siielewi, ”alisema Ngulumwa.
Kuruthumu Majjid alimfikisha Kituo cha Polisi Magomeni aliyekuwa akifanya naye biashara kwa madai alimdhulumu fedha. Anasema kuwa ilimlazimu kutoa chochote ili akamatwe na polisi na afikishwe kortini.
Alisema awali alipoambiwa ili mtuhumiwa akakamatwe lazima atoe fedha, alikataa. Baadaye alisalimu amri akatoa kiasi cha Sh80,000 lakini akaambiwa afikishe Sh100,000 na alipotekeleza, ndipo mdaiwa alipokamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni. Hata hivyo, mshitakiwa yuko nje kwa dhamana.
“Kuanzia hapo amekuwa akiwatambia watu kuwa ataniyumbisha sana katika kesi hii, na kweli hafiki mahakamani, huu ni mwezi wa 13 tangu nimshtaki, nasota kutwa nzima, kesi imesogezwa mbele zaidi ya mara nne, nahisi wanataka nichoke kesi ifutwe kinyemela, ”alisema.
Katika Mahakama ya Mbagala-Kizuiani, Abdallah Mjata analalamika kwamba amefungua kesi ya wizi wa kuaminiana muda mrefu lakini anazungushwa kila siku uchunguzi haujakamilika. Tofauti na siku nyingine sasa anatakiwa kumaliza kesi hiyo nje ya mahakama.
“Hapa unaponiona najipanga kuweka wakili. Kesi niliyofungua inamhusu jamaa niliyempa fedha, tukaandikishiana, kila kitu ninacho. Kinachofanyika hapa sikielewi kwani sijawahi kukutana na hakimu wala kesi kutajwa, nikija nakutana na hawa wanaojifanya wazee wa baraza na kuniomba nimalizane na mtuhumiwa, mimi sitaki ndiyo maana nasubiri kusonga mbele, ” alisema Mjata.
Mjata anadai kuwa kinachotembea kortini ni fedha kwamba hiyo ni tabia ya wanaojifanya watu wa kati ambao wanaharibu sura nzima ya kesi ndiyo maana anataka kuikomesha kwa kusonga mbele. “Siishii hapa kwa sababu nina faili, nilifungua kesi hapa,” anasisitiza.
Mzee mmoja wa baraza mahakamani hapo alikiri kuwapo watu wanaojifanya washauri wa mahakama wakati si wafanyakazi na hao ndiyo huchafua jina lao kwa kuwa watu wa kati wanakula fedha ya huku na huku. Alishauri watu wanaokuwa na kesi wasipende vitu rahisi kwa kuamini misaada midogomidogo na ahadi hewa ambazo hazitekelezi.
“Watu wajue kuna matapeli wengi wanaoishi mahakamani, hao wakigundua hilo wanajiweka kati, hivyo nashauri wahusika kuwa makini, hakuna kitu rahisi wala cha mkato zaidi ya kufuata sheria, vinginevyo wakikubali kulaghaiwa kirahisi watapata shida,” alisema mzee huyo ambaye hakutaja jina lake litajwa gazetini.
Mwanamke mmoja aitwaye Halima Abdan anasema ameliwa zaidi ya Sh1.2milioni huku akiwa hajafanikiwa kumtoa ndugu yake aliyepo mahabusu Segerea.
Halima aliangukia kwenye mikono ya askari ambaye hajawahi kukutana naye bali huzungumza naye kwenye simu baada ya kuunganishwa na mzee wa baraza akidai kuwa atamsaidia kumtoa ndugu yake aliyeko mahabusu kwa mwaka wa pili sasa.
Mara ya kwanza alitaka apewe Sh800,000 kwa madai kuwa siku atakapopelekwa kortini kwa ajili ya kusikilizwa kesi yake angeachiwa lakini ikashindikana. Mara ya pili alitaka apewe Sh300,000 ili agawane na askari wa Segerea na Sh100,000 kwa ajili ya kuwapa baadhi ya watu hapa mahakamani ili atoke lakini ilishindikana pia.
Halima anasema, ndugu yake hakufanya kosa ili alikumbwa na kesi hiyo kwa kuwa mtu aliyemdhamini amekimbia, hivyo akakamatwa na ameshakaa ndani karibu mwaka na nusu.
“Nikimtazama alivyokonda anapokuja mahakamani na tunapokwenda kumwona Segerea, natamani nifanye kitu chochote kumtoa. Niliwahi kukutana na hakimu mmoja akaniambia atanisaidia lakini naye amekula fedha na kila tukimpigia simu haipatikani tena na wala hatumuoni tena,” alisema.
Mtu mwingine aliyedakwa na mtandao wa kitapeli mahakamani ni Laizer Kaanan ambaye anasema ndugu yake amewekwa mahabusu Keko zaidi ya mwaka mmoja u na wanapotaka kumtoa “wanavunwa” fedha tu na wajanja wakiwamo mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo.
“Nimekuja nimwone, akishushwa tu naondoka najua kesi yake haitatajwa, kila siku ni hivyohivyo. Nimetoa karibu Sh600, 000, kila siku natajiwa fedha na mtu hatoki, nimechoka naona kuna watu wananifanya mrija wa kufyonza, akitoka sawa asipotoka basi, taratibu zote za dhamana nimekamilisha wamekaa nazo wao, badala ya kuzifanyia kazi wananifanya mtaji wa kuchumia, sitoi tena,” Kanaan alisema kwa masikitiko mahakamani hapo.
Katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kuna watu wa makamo huwa na makabrasha yenye nyaraka, ambao inadaiwa wanatumiwa na mahakimu na polisi kushawishi wenye mashauri watoe fedha kwa madai ya kufanikishiwa mambo yao.
“Wapo wengi; mahakimu na polisi wanashirikiana na matapeli hao; wengine wanafanikiwa kuwatoa jamaa zao mahabusu, kufuta kesi na kuwakandamiza wenye haki. Mtandao huo upo sana hapa,”anasema mzee mmoja maarufu eneo hilo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Claudiana Mbazigwa anasema kuwa ameliwa na wajanja kiasi cha Sh1.4 milioni kwa ajili ya kutaka ndugu yake aliyeko mahabusu ya Segerea atoke.
“Sasa karibu tunafilisika maana alipokuwa mahabusu Msimbazi wanaojifanya watu wa msaada walitaka tutoe Sh300,000, nikatoa. Lakini mpaka sasa ikiwa imepita zaidi ya miezi mitatu. Kila akiletwa hapa mahakamani tunaitwa kwa ajili ya kumwona angalau kwa mbali pamoja na kuonana na hao wanaodai kutusaidia kumtoa ambao tulifahamiana nao tangu akiwa Msimbazi. Hadi huku wanatutisha ili tutoe fedha, siku zinakwenda hakuna kinachofanyika,” anasema Mbazigwa.
Kisa cha kusikitisha zaidi kimempata Abdallah Mpondela aliyetoka Lindi kuja kushughulikia kesi ya ndugu yake na ikiwezekana kumtoa mahabusu. Baada ya kukamilisha taratibu zote za dhamana na kutoa Sh500,000 bado hajafanikiwa kumtoa.
“Kila nikija nakutana na wazee ambao hunieleza hali ya kesi na kunitaka nitoe fedha zaidi, labda tutafanikiwa kumtoa, nimeshatumia 980,000, hajatoka na leo alikuja hapa mahakamani..... kesi yake haijatajwa, sijui kwa nini. Hao wazee wamesema niwasubiri na sasa wamesema niwakute kwenye mgahawa wa Falcon ndiyo naenda kuutafuta,” alisema Mpondela.
Msajili wa Mahakama Kuu
Mahakimu wafawidhi wa mahakama hizo hawakupatikana na waliokuwa wanakaimu walidai hawana mamlaka ya kusemea jambo hilo zito. Lakini Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania, John Kahyoza anasema anayetakiwa kupinga rushwa ni mtoa rushwa, hivyo watumie njia mbalimbali za kupinga ikiwamo kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili kupata fedha kwa ajili ya kuwakamata wahusika.
Alisema kwa upande wao kama wasimamizi wa mahakama wana upelelezi maalumu wenye lengo la kuwafuatilia mahakimu wanaojihusisha na rushwa na wamewahi kuwakamata mara kadhaa na kuwachukulia hatua.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema kuwa wanajitahidi kupambana na rushwa lakini wanapata tatizo la ushahidi.
Post a Comment